top of page

AFUNGWA JELA MIAKA 30 KWA KUBAKA MTOTO WA MIAKA

Na Ester Madeghe


Mkazi wa Kijiji cha Nyehunge, Wilaya Sengerema mkoani Mwanza, Nicholaus Paulo Kidoganya (21) amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mtoto wa miaka mitano (jina linahifadhiwa) kwa sababu za kisheria.


Katika kesi hiyo ya Jinai namba 3239/2025, Kidoganya ametiwa hatiani na Mahakama ya wilaya Sengerema kwa kosa la kumbaka mtoto huyo. Hukumu hiyo imesomwa leo Februari 6,2025 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Sengerema, Evod Kisoka mbele ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali Mkaguzi wa Polisi, Nyamhanga Tissoro.


Awali, Mwendesha Mashtaka aliieleza Mahakama kwamba mshtakiwa alitenda kosa hilo Disemba 23, 2024, katika Kijiji cha Nyamadoke, wilaya ya Sengerema, mkoa wa Mwanza kinyume na vifungu vya 130(1)(2)(a) pamoja na kifungu cha 131(3) cha sheria ya kanuni ya Adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.


Mshtakiwa amefikishwa Mahakamani kwa mara ya kwanza leo 06.02.2025 na kusomewa shtaka hilo, kwa hiari yake bila kuisumbua mahakama aliamua kukiri kutenda kosa la kumbaka mtoto huyo.


Akieleza kwa upana mbele ya mahakama kuhusu kukiri kwake, mtuhumiwa alieleza kuwa siku ya tukio alimshawishi mtoto huyo kwa kumhahidi kumpa maembe yaliyokuwa juu ya mti wa maembe uliokuwa kwenye shamba la mahindi.


Baada ya mhanga kufika eneo hilo alimkamata na kumuingilia kimwili mpaka alipokutwa na kukamatwa na mwalimu wa shule ya msingi Nyamadoke iliyo karibu na eneo hilo (jina la mwalimu limehifadhiwa) akiwa anafanya kitendo hicho cha ubakaji.


Baada ya Mahakama kupitia vifungu vya sheria na ushahidi uliowasilishwa na upande wa Jamhuri ikiwemo ripoti ya Mganga aliyemfanyia uchunguzi mtoto huyo, pamoja na cheti cha kuzaliwa cha mhanga, Mahakama imejiridhisha bila ya kuacha shaka kwamba mtuhumiwa alitenda kosa hilo licha ya ukiri wake.


Baada ya kutiwa hatiani mshtakiwa aliiomba Mahakama imuachilie huru kwa kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na kudai kuwa alipitiwa na shetani. Akisoma hukumu hiyo Hakimu, Kisoka alimuhukumu mshtakiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama ya Nicholaus Kidanganya.

Comentarios


Msasa Media
  • Instagram
  • Facebook
  • X
  • Youtube
  • TikTok

Follow, like, comment, and share

Tel. +255758379300
Mbezi Dar es saalam

bottom of page