Na VENANCE JOHN
Polisi nchini Kenya wamemkamata mwanaume aliyetambulika kama John Kiama Wambua aliyekuwa amebeba sehemu za mwili wa maiti iliyokatwakatwa na kuwekwa kwenye begi la mgongoni.
![](https://static.wixstatic.com/media/57c8da_0a0043725ebf42d7b36996128b5e5550~mv2.jpeg/v1/fill/w_980,h_980,al_c,q_85,usm_0.66_1.00_0.01,enc_avif,quality_auto/57c8da_0a0043725ebf42d7b36996128b5e5550~mv2.jpeg)
Maafisa walikutana na John Kiama Wambua mwenye umri wa miaka 29, walipokuwa wakifanya doria eneo la Huruma, wilaya ya mashariki mwa Nairobi, kabla ya mapambazuko. Baada ya maafisa wa polisi kumhoji Wambua, aliwaambia viungo hivyo vya mwili ni vya mkewe, Joy Fridah Munani aliyekuwa na umri wa miaka 19.
Taarifa kutoka Ofisi ya Upelelezi wa makosa ya Jinai nchini Kenya (DCI), inasema polisi hao walimshuku Wambua kuwa amebeba kitu kisicho halali, walipekua begi lake na kwa mshtuko walikuta sehemu za mwili. Baada ya kuhojiwa, Wambua aliwaongoza maafisa hao hadi nyumbani kwake, ambapo waligundua kisu, nguo zilizolowa damu na viungo vingine vya mwili chini ya kitanda.
Ripoti ya DCI inaeleza kuwa mshukiwa atashtakiwa rasmi kwa mauaji mahakamani. Kenya ni mojawapo ya nchi zenye kiwango kikubwa cha mauaji ya wanawake barani Afrika kwani kwa mujibu wa Polisi wa Kenya kati ya Agosti na Oktoba mwaka jana, wanawake wasiopungua 97 wameuawa.
Comments