top of page

"ASANTE SANA MAMA SAMIA, NIMEFARIJIKA SANA",

- MBUNIFU WA GARI ATOA YA MOYONI Na Derek MURUSURI, Dar es Salaam26 Machi, 2024 ASANTE SANA MAMA SAMIA," ndiyo maneno aliyosema mbunifu Godfrey Charles, machozi yakimlenga lenga kwa furaha .

Kijana huyu Mbunifu mwenye umri wa miaka 26, hakuamini macho yake, pale taasisi za Serikali zinazosimamia bunifu, zilipomtembelea hadi nyumbani anakoishi, huko Kitunda. Hakuamini.

Msafara wa COSTECH na Kiwanda cha Magari cha NYUMBU cha Kibaha, walimtafuta kijana huyu mara tu baada ya habari za bunifu yake kutapakaa katika Mitandao ya ndani na nje ya



nchi. "Kama Serikali ya Mama Samia inafanya kazi kwa haraka na ufanisi wa aina hii, Vijana wenye ubunifu watafika mbali sana kwenye nchi hii," alisema Ishaka Issa, mkazi wa Kitunda aliyekuja kushuhudia ukaguzi wa gari hilo. Mkurugenzi Mkuu wa Tume inayoratibu bunifu za Sayansi Tanzania (COSTECH) Dkt. Amos NUNGU, mara tu baada ya habari za kijana aliyeunda gari mwenyewe kusambaa katika mitandao ya kijamii, hakuchekewa. Aliituma timu yake ikakutane na mbunifu huyo mara moja na kuona namna ya kumsaidia ili afikie ndoto yake na ubunifu wake kumfaidisha yeye mwenyewe, Vijana wa Tanzania na kuinua taswira na uchumi wa Tanzania.

Dkt. Athman Mgumia na Mhandisi Emmanuel Girimwa wa COSTECH, walifika na kulikagua gari hilo lililojengwa kwa asilimia 70 ya vifaa asilia na asilimia 30 ya vifaa vya nje vilivyoongezewa thamani. Mhandisi Tuntufye Kyusa kutoka Tanzania Automotive Technology Centre (Nyumbu) na Mhandisi mwenzake pia walifika katika ukaguzi wa gari hili, lililotengenezwa kwa injini ya pikipiki, iliyoboreshwa kwa vifaa vingine vya gari. Japo wengine husema bunifu hiyo ni pikipiki ya miguu minne, kwa vile imetumia injini ya pikipiki, wanasahau kuwa gari sio injini Bali umbo. "Ukiweza machine ya kusaigia kwenye trekta, haiitwi trekta, hali kadhalika ukijenga gari ukaweka injini ya pikipiki iliyoboreshwa kwa kuwekewa vifaa vya gari, hiyo sio pikipiki,' alisema Bw Issa na kuongeza kuwa, Watanzania wajifunze kuwapa moyo Vijana wabunifu ili wakue na kuubadilisha uchumi wa Taifa letu. "Ninazishukuru sana taasisi hizi za umma kwa mwitikio wao wa haraka sana baada ya kuona taarifa zangu mtandaoni. Asante sana Rais wangu na wasaidizi wako. Nimetiwa moyo. Asante sana Mama," alisema kijana huyo mbunifu kutoka Karagwe, mkoani Kagera.

Godfrey Charles ambaye ni fundi wa magari, amejipambanua kuwa na uthubutu wa KUJENGA gari kwa mikono yake, akianza na uchoraji wa gari hilo hadi ujenzi wake.

"Iwapo Tanzania chini ya Mama Dkt. Samia itafanya kazi kwa haraka jinsi hii, wakawaibua na kuwajenga vijana wabunifu, sio siku nyingi tutaanza kuuza magari, pikipiki, Bajaj na vyombo vya usafiri vilivyoundwa hapa hapa nchini na kuifikia Tanzania ya viwanda," alisema Godson Mbilinyi wa Msasa Online Media. Gari hiyo inatumia mafuta ya petroli.

Mbunifu Godfrey Charles aliibuliwa na *Msasa Online Media pamoja na Simon Woodgreen wa Afrimax, wa nje ya nchi, ambaye alimwita mbunifu huyo Elon Musk wa Tanzania.

Tanzania imejaa neema. Sio neema ya madini, gesi na mafuta pekee, bali hadi neema ya raslimali watu, waliobarikiwa kwa vipaji vingi na vya aina mbalimbali.

"Tunamwombea Mama Dkt. Samia afya njema na mafanikio makubwa sana anapohakikisha Vijana wabunifu kama hawa anawapatia vitendea kazi ili wafanye mambo makubwa kama alivyosema kwenye Citizen Rising Woman ya Mwananchi," alisema Ishaka na kumalizia, "Asante Mama, hakika unaijenga upya Tanzania yetu."

MWISHO.

Comments


Msasa Media
  • Instagram
  • Facebook
  • X
  • Youtube
  • TikTok

Follow, like, comment, and share

Tel. +255758379300
Mbezi Dar es saalam

bottom of page