top of page

DAWASA YASHIRIKI KONGAMANO LA KISAYANSI, DKT MPANGO ATAKA MATUMIZI YA AKILI MNEMBA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeshiriki Kongamano la nne la Kisayansi la maji linalofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Januari 29-31, 2025 lenye kauli mbiu ya "Suluhisho la Maji na Usafi wa Mazingira katikati ya Mabadiliko ya Tabianchi".


Kongamano hilo lililoandaliwa na Chuo cha Maji limekutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya Maji wakiwemo wa Serikali na sekta binafsi kwa lengo kujadiliana mikakati ya kukabiliana mabadiliko ya Tabianchi.


Mgeni rasmi alikuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ambaye kwenye hotuba yake

amesisitiza umuhimu wa kubuni mifumo na mbinu za kutunza vyanzo vya maji na ardhi oevu, akieleza matumizi ya maji kwa binadamu, mifugo, na wanyamapori yanapaswa kuzingatiwa kwa usawa.


Dk Mpango amewataka wataalamu wa sekta ya maji, hususan wa Chuo cha Maji, kutumia Teknolojia ya akili mnemba (AI) katika kutafuta suluhisho la changamoto za maji na usafi wa mazingira.


"Ninawaomba, hasa wenzetu wa Chuo cha Maji, tumieni akili mnemba (AI) kila inapowezekana katika kutafuta suluhisho la changamoto za maji na usafi wa Mazingira. Pia mshirikishe vijana bunifu wa Kitanzania na nchi nyingine za Afrika," amesema.


Makamu wa Rais amesema: "Mabadiliko ya tabianchi yanazidi kuathiri utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, hususan lengo namba sita linalohusu maji na usafi wa mazingira. Ukame na mafuriko yanayosababishwa na mabadiliko haya siyo tu yanapoteza maisha ya wananchi wetu, bali pia yanaharibu miundombinu na kusababisha upungufu wa chakula."


Awali, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso amesema Wizara ya Maji imeanzisha Kampuni ya Ushauri ya Water Institute Consultancy Bureau Limited ili kutumia wataalamu waliostaafu kuwajengea uwezo vijana wanaoingia katika Sekta ya Maji.


"Tunataka kuona Chuo cha Maji kikizalisha wataalam mahiri, wachapakazi na wenye uwezo wa kufanya tafiti za kina zinazoweza kutatua changamoto za maji na usafi wa mazingira nchini," amesema Waziri Aweso.


Kongamano hilo litafanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 29 hadi 31 Januari, 2024.

Comments


Msasa Media
  • Instagram
  • Facebook
  • X
  • Youtube
  • TikTok

Follow, like, comment, and share

Tel. +255758379300
Mbezi Dar es saalam

bottom of page