Na VENANCE JOHN
Hatimaye Yoon Suk Yeol rais wa Korea Kusini amekuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo aliyeko madarakani kukamatwa. Kukamatwa kwake, kumemaliza mzozo uliodumu kwa wiki kadhaa kati ya wachunguzi na waendesha mashtaka kwani mara kadhaa walishindwa kumkamata baada ya rais huyo kukaidi wito wa kufika mbele ya wachunguzi kwa ajili ya kuhojiwa.
![](https://static.wixstatic.com/media/57c8da_069dca093e564f00971ae11349489e00~mv2.jpeg/v1/fill/w_980,h_980,al_c,q_85,usm_0.66_1.00_0.01,enc_avif,quality_auto/57c8da_069dca093e564f00971ae11349489e00~mv2.jpeg)
Yoon, ambaye jaribio lake lilishindwa la kuweka sheria ya kijeshi liliitumbukiza nchi hiyo katika msukosuko na kumwona rais Yoon akishtakiwa na bunge, na sasa anachunguzwa kwa tuhuma za uasi (uhaini). Hata hivyo, kitaalamu bado ni rais kama mahakama ya kikatiba inapaswa kuamua kama kushtakiwa kwake ni halali.
Wachunguzi walilazimika kutumia ngazi na vikata nyaya kwenye baridi kali ili kumfikia Yoon, ambaye wafanyakazi wake wa Idara ya Usalama wa Rais (PSS) walikuwa wameweka vizuizi kwa nia ya kuzuia kukamatwa kwake. Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 64 amesema amekubali kufika mbele ya Ofisi ya Uchunguzi wa Ufisadi kwa maafisa wa ngazi za juu (CIO) ili kuepuka umwagaji damu.
Katika ujumbe wa video wa dakika tatu, Yoon amesema atazingatia uchunguzi dhidi yake ingawa alikuwa anaupinga. Amekuwa akishikilia kuwa hati ya kukamatwa kwake sio halali kisheria. Zaidi ya maafisa 1,000 walikuwa sehemu ya operesheni ya alfajiri ya leo Jumatano ambayo ilikuwa mara ya pili kwa maafisa kujaribu kumkamata.
Nchi hiyo kwa sasa inaongozwa na Waziri wa Fedha Choi Sang-mok kama kaimu rais. Aliingizwa madarakani baada ya kaimu rais wa kwanza, Han Duck-soo, pia kushtakiwa na bunge la wengi la upinzani. Iwapo mahakama haitatoa kibali cha kuzuiliwa ndani ya saa 48 baada ya Yoon kukamatwa, hata hivyo, ataachiliwa, na kuwa huru kurejea katika makao ya rais.
Comments