Na VENANCE JOHN
Baraza la usalama la taifa nchini Iran limesitisha utekelezaji wa sheria ya hijabu na kutokuwa na mahusiano yoyote ya ngono kabla ya ndoa, ambayo ilitakiwa kuanza kutekelezwa Ijumaa ya wiki hii. Rais Massoud Pezeshkian aliita sheria hiyo kuwa yenye utata na kwamba ilihitaji marekebisho. Tamko hilo liliashiria nia ya rais Massoud Pezeshkian kutathmini upya hatua zake.
Sheria mpya iliyopendekezwa ingeleta adhabu kali zaidi kwa wanawake na wasichana kwa kutofunika nywele zao, kuonyesha mapaja au sehemu ya chini ya miguu. Sheria hiyo ilikuwa imekosolewa vikali na wanaharakati wanaotetea haki za binadamu.
Kanuni kali za mavazi zilizowekwa kwa wanawake na wasichana, ambazo zimechukuliwa kama kipaumbele cha usalama wa taifa na watawala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa miongo kadhaa, zimekuwa zikisababisha maandamano siku za nyuma.
Chini ya sheria hiyo mpya, wahalifu wanaorudia makosa na yeyote aliyekejeli sheria hizo atakabiliwa na faini kubwa zaidi na kifungo cha muda mrefu cha hadi miaka 15 jela. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, vijana wengi wa kike wa Irani wamekuwa wakivua hijabu zao kwa ukaidi hadharani, wakipinga mamlaka ya serikali.
Comentarios