Na Ester Madeghe,
Jeshi la Israel limetoa ripoti inayowashutumu waandishi wa habari kadhaa, kwa kuwa na uhusiano na Hamas pamoja na makundi ya Kiislamu ya Palestina. Madai ya siku za hivi karibuni dhidi ya waandishi wa habari wa Al Jazeera huko Gaza ni sehemu ya mwenendo unaosumbua wa jeshi la Israel.

Al Jazeera imekataa kwa uthabiti madai hayo, huku vikundi vya Wapalestina vinavyofuatilia ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya waandishi wa habari vikiibua wasiwasi mkubwa. Vikundi hivyo vinavyotetea haki za waandishi wa habari, vinasema kwamba, madai hayo "yanatishia moja kwa moja usalama na maisha ya wanahabari wanaohusika".
Katika mwaka uliopita, karibu waandishi wa habari 200 wa Kipalestina wameuawa huko Gaza, wakiwemo waandishi habari kutoka Al Jazeera katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu. Kadhalika, zaidi ya waandishi wa habari 120 wamekamatwa na mamlaka ya Israel, na 52 bado wamefungwa.
Wengi wa wanahabari hawa wanakamatwa kwa sababu tu ya kuwa waandishi wa habari au kwa kuchapisha habari mtandaoni kwenye mitandao ya kijamii, ambapo mpaka sasa hakuna mwandishi yeyote wa habari aliyeshutumiwa kwa uhalifu wowote.
Israel inaendelea kupiga marufuku operesheni za Al Jazeera katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na mashambulizi yaliyolengwa dhidi ya waandishi wa habari huko Gaza. Ambapo ripoti ya hivi punde inaonesha ongezeko la hatari kubwa ambazo wanakabiliana nazo waandishi wa habari katika kanda hiyo.
Comments