Na VENANCE JOHN
Mashambulizi ya anga ya Israel yamewauwa takriban watu 70 huko Gaza usiku wa kuamkia leo Alhamisi. Wakaazi na mamlaka katika eneo hilo wamesema, tukio hilo limetokea saa chache baada ya kutangazwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano na kuwaachilia mateka ili kumaliza vita vya miezi 15 kati ya Israel na Hamas.
Baadhi ya Wapalestina wanataka makubaliano hayo yatekelezwe kwa haraka zaidi. Wakati watu wakisherehekea mapatano hayo huko Gaza na Israel, jeshi la Israel lilifanya mashambulizi zaidi na watu 71 kuuliwa na wengine karibu 200 kujeruhiwa.
Makubaliano ya kusitisha mapigano yalifanyika jana Jumatano baada ya upatanishi kati ya Qatar, Misri na Marekani ya kusitisha vita ambavyo vimeharibu eneo la pwani na kuchochea machafuko katika eneo la Mashariki ya Kati. Makubaliano hayo, yaliyopangwa kutekelezwa kuanzia Jumapili, yanaainisha usitishaji vita wa wiki sita wa awali na kuondolewa taratibu kwa vikosi vya Israel kutoka Ukanda wa Gaza.
Mateka waliochukuliwa na kundi la wanamgambo wa Hamas, ambalo linadhibiti eneo hilo, wataachiliwa kwa kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina wanaozuiliwa na Israel. Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameshutumu Hamas kwa kukiuka matakwa ya makubaliano.
Comentarios