Na VENACE JOHN
Shirika la ulinzi wa data la Italia leo limesema kwamba limeitoza faini ya euro milioni 15 sawa na dola milioni 15.58 OpenAI ambayo ni kampuni mtengenezaji wa program ya akili mnemba ya ChatGPT baada ya uchunguzi wa matumizi ya data ya kibinafsi.
Faini hiyo inakuja baada ya mamlaka hiyo kuipata kampuni ya OpenAI ilichakata data binafsi za watumiaji ili kuifundisha ChatGPT bila kuwa na msingi wa kutosha wa kisheria na kukiuka kanuni ya uwazi na wajibu wa habari kuhusiana na watumiaji. OpenAI imesema uamuzi huo haukuwa na uwiano sawa na kwamba kampuni itawasilisha rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Uchunguzi huo, ulioanza mwaka wa 2023, pia ulihitimisha kuwa kampuni hiyo yenye makao yake makuu nchini Marekani haikuwa na mfumo wa kutosha wa kuthibitisha umri ili kuzuia watoto walio chini ya umri wa miaka 13 kuonyeshwa maudhui yasiyofaa yanayotokana na akili mnemba (AI).
Shirika la uangalizi la Italia pia limeamuru OpenAI kuzindua kampeni ya miezi sita kwenye vyombo vya habari vya Italia ili kuhamasisha umma kuhusu jinsi ChatGPT inavyofanya kazi, hasa kuhusu ukusanyaji wa data ya watumiaji na wasio watumiaji kutoa mafunzo ya algoriti (Algorithism).
Mamlaka ya Italia, inayojulikana kama Garante, ni mmoja wa wadhibiti mahiri wa Umoja wa Ulaya katika kutathmini ufuasi wa jukwaa la akili mnemba na utaratibu wa faragha wa data. Mwaka jana ilipiga marufuku kwa ufupi matumizi ya ChatGPT nchini Italia kwa madai ya ukiukaji wa sheria za faragha za Umoja wa Ulaya.
Huduma ilianzishwa upya baada ya OpenAI inayoungwa mkono na Microsoft kushughulikia masuala yanayohusu, miongoni mwa mambo mengine, haki ya watumiaji kukataa kibali cha matumizi ya data ya kibinafsi kutoa mafunzo kwa algoriti (Algorithism).
Comments