Na VENANCE JOHN
Waendesha baiskeli wanaotumia simu na kuvaa spika za masikioni (earphone) nchini Japan wanaweza kufungwa jela hadi miezi sita chini ya sheria mpya iliyoanza kutumika leo Ijumaa. Wale wanaokiuka sheria ya barabarani wanaweza kuadhibiwa kwa kifungo cha juu zaidi cha miezi sita gerezani, au faini ya Yen 100,000 sawa na dola za Marekani 655 (zaidi ya Tsh 1,768,500).

Kando na kutaka kufifisha matumizi ya simu, sheria hizo mpya pia zinalenga waendesha baiskeli wanaoendesha wakiwa wamekunywa pombe, kupewa adhabu ya hadi miaka mitatu jela au faini ya Yen 500,000 ambayo ni dola za Marekani 3,278 ( zaidi ya Tsh 8,850,600).
Idadi ya ajali zinazohusisha waendesha baiskeli zilianza kupanda mwaka 2021, kwani watu wengi walichagua kuendesha baiskeli badala ya kutumia usafiri wa umma wakati wa janga la CORONA. Mwezi Mei, bunge la Japan lilipitisha mswada unaowaruhusu polisi kuwatoza faini waendesha baiskeli kwa ukiukaji wa sheria za barabarani
Kulingana na vyombo vya habari vya ndani, zaidi ya ajali 72,000 za baiskeli zilirekodiwa nchini Japani mwaka wa 2023, zikichukua zaidi ya 20% ya ajali zote za barabarani nchini humo. Mwaka jana, mamlaka ilifanya kuwa lazima kwa waendesha baiskeli kuvaa kofia ngumu (helmet).Sheria hizi zinakuja zikilenga kulinda usalama wa wasafiri na watembea kwa miguu.
Comments