Na VENANCE JOHN
Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Geita imemhukumu kifungo cha miaka 15 jela, Andrea George mwenye umri wa miaka 21 kwa kosa la kumuua mke wake, Tabu Jems bila kukusudia. Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kelvin Mhina baada ya kusikiliza kesi hiyo iliyokuja mahakamani hapo leo Januari 20, 2025 kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali.
![](https://static.wixstatic.com/media/57c8da_e5e0211d11164e12ba79aceebae4e234~mv2.jpeg/v1/fill/w_980,h_980,al_c,q_85,usm_0.66_1.00_0.01,enc_avif,quality_auto/57c8da_e5e0211d11164e12ba79aceebae4e234~mv2.jpeg)
Mwendesha mashitaka wa Serikali, Wakili Scolastica Teffe akisoma maelezo ya awali ya mshtakiwa, ameieleza Mahakama kuwa Juni 13, 2024 katika kijiji cha Nyakahengele B kata ya Ihanamilo wilayani Geita, mshtakiwa alimuua mkewe bila kukusudia kinyume na kifungu cha 195 na 198 cha kanuni ya adhabu kilichofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Ameieleza Mahakama kuwa siku ya tukio marehemu Tabu Jems akiwa na mdogo wake Naomi wakitokea eneo la Nyakahengele A walikutana na mshtakiwa ambaye aliomba kuzungumza na mkewe (Tabu) kwa kuwa walikua wameachana, mkewe aligoma kwenda kuzungumza naye.
Amedai baada ya mkewe kukataa mshtakiwa alitoa panga alilokuwa ameficha kwenye nguo na kuanza kumshambulia nalo sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo kichwani, shingoni na kwenye mikono hali iliyosababisha kifo chake.
Mdogo wa mke wake alikimbia na kuomba msaada kwa majirani ambao walifika na kutoa taarifa polisi na polisi walipofika waliuchukua mwili na kumkamata mshtakiwa aliyekua amejificha kwenye nyumba ya jirani,” ameeleza Teffe. Kutokana na maelezo hayo mshtakiwa alikiri kuua bila kukusudia na kutiwa hatiani.
Commentaires