Na VENANCE JOHN
Jenerali mkuu wa Urusi anayetuhumiwa na Ukraine kwa kuhusika na matumizi ya silaha za kemikali dhidi ya wanajeshi wa Ukraine ameuawa mjini Moscow.

Ukraine imesema mauaji ya kamanda mwandamizi wa jeshi la Urusi, Igor Kirillov, mjini Moscow yalitokana na Operesheni maalumu iliyofanywa na idara ya ujasusi ya Ukraine - SBU. Wachunguzi wa Urusi leo wameeleza kuwa Igor Kirillov ameuawa kwa kutumia bomu lililofichwa kwenye baiskeli ya umeme (scooter).
Luteni Jenerali Igor Kirillov, ambaye alikuwa mkuu wa Kikosi cha Kulinda Nyuklia, Biolojia na Kemikali cha Urusi, aliuawa nje ya jengo la ghorofa huko Ryazansky Prospekt pamoja na msaidizi wake, Kamati ya Uchunguzi ya Urusi, ambayo inachunguza uhalifu mkubwa, ilisema katika taarifa.
Picha zilizochapishwa kwenye chaneli za Telegram za Urusi zilionyesha mlango uliovunjwa wa jengo lililotapakaa vifusi na miili miwili ikiwa kwenye theluji iliyotapakaa damu. Picha za shirika la habari la Reuters kutoka eneo la tukio zilionyesha kamba ya polisi. Urusi hata hivyo imesema italipa kisasi kufuatia kifo cha mkuu huyo wa silaha za kemikali na silaha za kibaiolojia.
コメント