NA VENANCE JOHN
Jimbo Kuu Katoliki jimbo la Nairobi limekataa na kurejesha mchango wa fedha kutoka kwa kwa Rais William Ruto na Gavana Johnson Sakaja, likisema halitaki kutumika kisiasa.
![](https://static.wixstatic.com/media/57c8da_ca367219fb8b4565ac99c379f9811980~mv2.jpeg/v1/fill/w_980,h_980,al_c,q_85,usm_0.66_1.00_0.01,enc_avif,quality_auto/57c8da_ca367219fb8b4565ac99c379f9811980~mv2.jpeg)
Askofu Mkuu Philip Anyolo, ambaye ndiye Askofu wa jimbo la Nairobi amesema kanisa Katoliki linapinga vikali matumizi ya matukio kama harambee na mikusanyiko mingine kama majukwaa ya kujitafutia umaarufu wa kisiasa. “Wanasiasa wanahimizwa kuepuka kugeuza madhabahu kuwa jukwaa la hotuba za kisiasa, kwani vitendo hivyo vinadhalilisha utakatifu wa maeneo ya ibada.” Amesema Askofu Anyolo.
Jumapili ya Novemba 17, 2024, Rais Ruto alitoa Ksh 600, 000 (sawa na Tsh12.3 milioni) kwa kwaya ya kanisa katoliki la Soweto na Baraza la Wamisionari wa Parokia. Pia alitoa Ksh 2 milioni (sawa na Tsh41.2 milioni) kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya padre, huku Gavana Sakaja akitoa Sh200,000 ( Tsh4.1 milioni).
Rais Ruto aliahidi kununua basi la parokia na kuongeza ahadi ya Sh3 milioni (TSh 61.6 milioni) nyingine kwa ujenzi wa nyumba ya kasisi. Askofu Anyolo amelitaka kanisa kudumisha uadilifu kwa kukataa michango inayoweza kuhatarisha uhuru wake au kusaidia kujitajirisha kwa njia zisizo za haki.
Amewahimiza viongozi wa kisiasa kuonyesha uongozi wa kimaadili kwa kushughulikia masuala nyeti yaliyoibuliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki wa Kenya (KCCB) kama migogoro ya kisiasa, ufisadi, siasa za ubinafsi, ukiukwaji wa haki za binadamu, na uhuru wa kujieleza.
“Kanisa lazima libaki kuwa chombo huru kisichohusishwa na ushawishi wa kisiasa, ili liweze kuhudumu ipasavyo kama mahali pa ukuaji wa kiroho na mwongozo wa jamii,” amesema Askofu Mkuu Anyolo katijka taarifa yake.
Hii inaenesha kuwapo na msuguano kati ya kanisa hilo na Rais Ruto kwani baada ya Baraza la Maaskofu Katoliki wa Kenya (KCCB) kuikosoa serikali ya Ruto wiki iliyopita, Naye Ruto alijibu kwa kulikosoa baraza hilo.
Comments