Na VENANCE JOHN
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameonya kwamba iwapo Marekani itaweka ushuru wa ziada kwa bidhaa za Umoja wa Ulaya (EU), watu wa Ulaya watajibu mapigo hapo hapo ndani ya saa moja.
![](https://static.wixstatic.com/media/57c8da_dabb3db071da49d088f644b59b2841b8~mv2.jpeg/v1/fill/w_980,h_980,al_c,q_85,usm_0.66_1.00_0.01,enc_avif,quality_auto/57c8da_dabb3db071da49d088f644b59b2841b8~mv2.jpeg)
Olaf Scholz amesema hayo katika mdahalo wa uchaguzi na Friedrich Merz, kiongozi wa chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union, akijibu maswali ya waandishi habari kuhusu uwezekano wa Trump kuzidisha ushuru wa forodha dhidi ya nchi za Ulaya.
Olaf Scholz ameongeza kuwa; "Sisi katika Umoja wa Ulaya tutachukua hatua ndani ya saa moja." Baada ya kuingia madarakani, Rais wa Marekani, Donald Trump amekuwa akiwatishia washirika wa nchi hiyo kuwawekea ushuru ziada wa bidhaa zao zinazoingizwa nchini Marekani.
Wiki iliyopita, alitangaza ushuru wa ziada dhidi ya China, Mexico na Canada, lakini saa kadhaa baadaye alitangaza kusimamishwa kwa mwezi mmoja ushuru wa ziada kwa Mexico na Canada lakini China ikaamua kujibu mapigo kwa kuweka ushuru wa asilimia 15 kwa bidhaa za Marekani.
Tume ya Ulaya pia ilikuwa imemuonya Trump kwamba Umoja wa Ulaya itatoa jibu kali kwa mshirika yeyote wa kibiashara ambaye anaweka ushuru usio wa haki au wa kiholela kwa bidhaa za jumuiya hiyo.
Comments