Naibu Waziri wa Nishati, Mhe Judith Kapinga amesema mafanikio yanayoonekana katika Sekta ya Nishati ni jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani ndiye anayetafuta fedha za kutekeleza miradi ya nishati nchini.

Mhe. Kapinga ameyasema hayo Novemba 07, 2024 Bungeni jijini Dodoma wakati akitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizotolewa na Wabunge wakati wa mjadala wa mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
"Miradi mingi inatekelezeka kwa sababu ya jitihada za Mheshimiwa Rais, huku Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akihakikisha kwamba miradi yote inatekelezwa kwa ufanisi na weledi mkubwa. Amesema Kapinga
Ameongeza kuwa, Sekta ya Nishati ina umuhimu mkubwa nchini kwani ni sekta wezeshi katika kuchangia ukuaji wa uchumi kupitia biashara, viwanda, kilimo pamoja na shughuli nyingine za kijamii.
Kapinga amesema katika kipindi chote cha utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo Sekta ya Nishati imejikita katika kuhakikisha inaboresha miundombinu ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme pamoja na kuboresha misingi ya kiuchumi katika sekta ya mafuta na gesi ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira wezeshi kwa kuhusisha sekta binafsi.
Amesisitiza kuwa wakati wa kuanza utekelezaji wa Mpango wa Taifa mwaka 2021 Nchi ilikuwa na megawati 1,571 za umeme kwenye gridi ya Taifa lakini utakapokamilika mradi wa umeme wa Julius Nyerere Nchi itakuwa na megawati 3,914.
Amesema mradi wa Julius Nyerere hivi sasa unazalisha megawati 940 kupitia mitambo minne na kuongeza kuwa ili kuwa na umeme mwingi zaidi Serikali inaangalia vyanzo vingine vya uzalishaji wa umeme.
Comments