top of page

KIKOSI CHA PILI CHA POLISI 200 WA KENYA CHAWASILI NCHINI HAITI Na VENANCE JOHN

Kikosi cha pili cha Askari polisi kutoka Kenya jana kimewasili nchini Haiti ambapo jukumu lao ni pamoja na kusaidia polisi wa Haiti kurejesha sheria na utulivu, kulinda miundombinu muhimu, na kuwezesha utoaji wa misaada ya kibinadamu.




Taarifa zinaeleza kuwa magenge yenye silaha yanadhibiti takriban 80% ya mji mkuu wa Haiti Port-au-Prince.

Kikosi hiki cha pili cha kina maafisa 200 wa polisi wa Kenya waliondoka Nairobi kuelekea Haiti mapema Jumanne kujiunga na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Msaada wa Usalama wa Kimataifa nchini Haiti.

Hizi ni juhudi zinazolenga kupambana na ghasia za magenge na kurejesha utulivu katika taifa hilo lililo ukanda wa Karibea.

Kulingana na taarifa ya pamoja ya mratibu wa misheni hiyo Noor Gabow na kaimu Naibu Inspekta Jenerali James Kamau wamesema maafisa hao, wametolewa kutoka vitengo maalum kama vile Kitengo cha Usambazaji Haraka (RDU) na Kitengo cha Huduma kwa Jumla (GSU), wameondoka kwa ndege ya kukodishwa na Umoja wa Mataifa

Kutumwa huko kunafuatia kikosi cha kwanza cha maafisa 400 wa polisi wa Kenya waliofika Haiti Juni 25, wakiwa na jukumu la kushughulikia ghasia za magenge zinazozidi kuongezeka ambazo zimeiingiza nchi hiyo katika janga la kibinadamu.

Polisi wa Kenya wataongoza ujumbe wa kimataifa, ambao unatarajiwa kujumuisha maafisa kutoka mataifa mengine katika wiki zijazo.

Nchi ya Haiti imekuwa ikipambana na ghasia za magenge na ukosefu wa utulivu wa kisiasa kwa miaka. Nchi hiyo ilishuhudia kuongezeka kwa ghasia kufuatia mauaji ya Rais Jovenel Moise miaka mitatu iliyopita.

Makundi hasimu yenye silaha yalichukua udhibiti wa mji mkuu, Port-au-Prince, mapema mwaka huu, na kumlazimisha Waziri Mkuu Ariel Henry kujiuzulu.

Mtaalamu wa maendeleo wa Umoja wa Mataifa Garry Conille aliteuliwa kuwa waziri mkuu mpya wa Haiti mwezi Mei kuchukua nafasi ya Ariel Henry baada ya kulazimishwa na magenge ya uhalifu kuachia ngazi.

Hozzászólások


Msasa Media
  • Instagram
  • Facebook
  • X
  • Youtube
  • TikTok

Follow, like, comment, and share

Tel. +255758379300
Mbezi Dar es saalam

bottom of page