Na VENANCE JOHN
Kiongozi wa chama cha upinzani hapa nchini cha ACT -Wazalendo Dorothy Semu ameweka wazi nia yake kugombea nafasi ya Urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2025. Semu amesema yuko tayari kukabiliana na Rais wa sasa wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Uchaguzi Mkuu wa 2025, iwapo chama chake kitampa ridhaa ya kufanya hivyo. Kulingana na kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo, kuna mapungufu nchini yanayohitaji uongozi thabiti, uwazi na malengo halisi kwa manufaa ya Watanzania wote.
Semu amebainisha kuwa iwapo atapewa ridhaa atahakikisha kuwa anapambana na kupanda kwa gharama za maisha, kuongeza kasi ya ukuaji uchumi, kushughulikia changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana pamoja na udhaifu katika usimamizi wa rasilimali za taifa.
Semu anakuwa mwanasiasa wa pili kutoka ACT-Wazalendo upande wa upinzani kutangaza azma ya kuwania nafasi ya juu kabisa ya uongozi nchini Tanzania, kwani mwaka 2015 Bi. Anna Elisha Mghwira aligombea nafasi hiyo akiwa ndani ya chama hicho.
ACT-Wazalendo ni chama cha kwanza kati ya vyama 19 vya siasa nchini Tanzania kuwaruhusu wananchama wake kutia nia na kutangaza kugombea uongozi katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka 2025 na ni chama ambacho kimekuwa kikitoa fursa kwa wanawake kushika wa ngazi za juu za uongozi wa chama.
Comentários