Na VENANCE JOHN
Korea Kaskazini imesema vikosi vyake vya kijeshi viko tayari kuchukua hatua zozote zinazohitajika baada ya manowari ya nyuklia ya Jeshi la Wanamaji la Marekani kutia nanga katika bandari ya mji wa Busan nchini Korea Kusini, na kuishutumu Marekani kwa tishio kubwa kwa usalama wa taifa lake.
![](https://static.wixstatic.com/media/57c8da_21ccf13e876a42eda6f7540b1e999f90~mv2.jpeg/v1/fill/w_980,h_980,al_c,q_85,usm_0.66_1.00_0.01,enc_avif,quality_auto/57c8da_21ccf13e876a42eda6f7540b1e999f90~mv2.jpeg)
Shirika la habari la serikali ya Korea Kaskazini KCNA siku ya leo limenukuu Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo ikisema katika taarifa yake kwamba kuwapo kwa manowari ya nyuklia ya Marekani kwenye Peninsula ya Korea ni maelezo ya wazi ya hali ya wasiwasi ya makabiliano dhidi ya Marekani.
"Tunaelezea wasiwasi mkubwa juu ya kitendo hatari cha uhasama cha Marekani ambacho kinaweza kusababisha makabiliano makali ya kijeshi katika eneo karibu na Peninsula ya Korea hadi kwenye mzozo halisi wa jeshi," ilisema taarifa hiyo.
Wizara hiyo ilisema Korea Kaskazini itatumia haki halali bila kusita kuwaadhibu wachochezi, kwa kuishutumu Marekani kwamba ni kikundi ambacho kinaamini kutawala kupitia mamlaka yake.
Manowari ya USS Alexandria ilitia nanga katika bandari ya Busan siku ya jana kwa ajili ya vifaa na kuwapa mapumziko wafanyakazi wake, kulingana na Wizara ya Ulinzi ya Korea Kusini. Korea Kaskazini inadai kuwa shughuli za kijeshi za pamoja kati ya Marekani na Korea Kusini ni tishio kwa amani kwenye Peninsula ya Korea, na inazichukulia kama mazoezi ya kuivamia Korea Kaskazini.
Comments