Na VENANCE JOHN
Majaji wawili wakuu wa Iran wameuawa katika shambulizi la risasi katika Mahakama ya Juu katika mji mkuu Tehran. Mauaji hayo yalitekelezwa na mtu mwenye silaha, ambaye alijiua baada ya kufyatua risasi.
![](https://static.wixstatic.com/media/57c8da_41af3c9282e54991ad9913ad970e4bfb~mv2.jpeg/v1/fill/w_980,h_980,al_c,q_85,usm_0.66_1.00_0.01,enc_avif,quality_auto/57c8da_41af3c9282e54991ad9913ad970e4bfb~mv2.jpeg)
Kulingana na mahakama na vyombo vya habari vya serikali tukio hilo lilitokea mapema Jumamosi, siku ya kwanza ya kazi nchini Iran. Waliouawa walitambuliwa kuwa ni wanazuoni wa Kiislamu Ali Razini na Mohammad Moghiseh, wote wakiwa na cheo cha hujjat al-Islam na kila mmoja akisimamia tawi tofauti la mahakama hiyo.
Walishiriki kikamilifu katika kupambana na uhalifu dhidi ya usalama wa taifa, ujasusi na ugaidi na taarifa ya mahakama imeleza kuwa majaji waliouawa ni wajasiri na wazoefu. Msemaji wa mahakama Asghar Jahangir aliiambia runinga ya taifa ya Iran kwamba mtu mwenye bunduki aliingia ndani ya chumba cha majaji hao wawili na kuwapiga risasi.
Hata hivyo utambulisho wa mshambuliaji huyo mpaka sasa haujatambulika wala nia yake haikufahamika mara moja. "Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mhalifu hakuwa na kesi za awali katika Mahakama ya Juu.
Kwa mujibu wa gazeti la serikali la Tehran Times, mlinzi wa mmoja wa majaji hao pia alijeruhiwa katika shambulio hilo.Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian amesema kitendo hicho ni cha kigaidi na cha woga na kwamba lazima kifuatiliwe haraka na vikosi vya usalama na vyombo vya sheria.
Mkuu wa mahakama ya Iran Gholam-Hossein Mohseni Ejei amesema katika taarifa kwamba majaji hao waliuawa kutokana na hukumu zao dhidi ya magaidi ambao mikono yao ilikuwa imelowa damu ya watu wasio na hatia wa wa Iran.
Comments