top of page

MAKUMI YA RAIA WANAOIKIMBIA KOREA KASKAZINI WALIOKAMATWA NA POLISI WA SIRI WALITOWEKA; LINASEMA SHIRIKA LA KUTETEA HAKI ZA BINADAMU

Na VENANCE JOHN


Zaidi ya raia 100 wa Korea Kaskazini wametoweka baada ya kukamatwa na polisi wa siri walipokuwa wakijaribu kuihama nchi hiyo iliyotengwa na jumuiya ya kimataifa Shirika la kutetea haki za binadamu lenye makao yake mjini Seoul, Korea Kusini limesema katika ripoti yake ya leo Alhamisi kwamba watu hao hukamatwa pale wanapojaribu kuihama nchi yao au hata pale wanapojaribu kuwapigia simu jamaa zao walioko Korea Kusini.


Shirika hilo kwa jina la Transitional Justice Working Group (TJWG) limetoa ripoti inayoelezea mifumo ya upotevu uliotekelezwa kupitia utafiti wake kulingana na mahojiano na watu 62 waliotoroka kutoka Korea Kaskazini mpaka kufika nchini Korea Kusini.


Makumi ya maelfu ya Wakorea Kaskazini wamekuwa wakiikimbia nchi yao kwa miongo kadhaa tangu vita vya Korea hizo mbili vilipoisha mwaka 1953 huku wengi wa wale waliokamatwa au kurejeshwa makwao wakipelekwa kwenye kambi za magereza au vituo vingine vya kizuizini. Shirika hilo liligundua watu 113 katika kesi 66 walitoweka, pamoja na kesi zao kufutwa kwenye kumbukumbu


Kati ya watu 113, asilimia 80 mpaka 90, walikamatwa wakiwa ndani ya Korea Kaskazini na wengine wakiwa nchini China au Urusi, na takriban asilimia 30 walitoweka tangu kiongozi Kim Jong Un achukue madaraka mwishoni mwa 2011.


Mhojiwa aliyehamia Korea Kusini mwaka 2018 kutoka mji wa mpakani wa China wa Hyesan alisema rafiki yake alikamatwa alipokuwa akijaribu kusaka simu ya mkononi ya China iliyofichwa milimani, na sasa inasemekana kuwa amefariki.


Korea Kaskazini kwa muda mrefu imekuwa ikiwashutumu wanaoikimbia nchi hyo kama "takataka za binadamu", na kiongozi wake Kim Jong-Un ameimarisha zaidi udhibiti wa mpaka katika miaka michache iliyopita.

Comments


Msasa Media
  • Instagram
  • Facebook
  • X
  • Youtube
  • TikTok

Follow, like, comment, and share

Tel. +255758379300
Mbezi Dar es saalam

bottom of page