Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), ametoa wito kwa Watanzania, hususan wale wanaojihusisha na shughuli za uvuvi kulinda rasilimali hizo za asili ili kuwahakikishia wananchi kukuza uchumi wao kwa misingi endelevu na kuwahakikishia upatikanaji wa malighafi (samaki) wawekezaji wa sekta binfasi waliowekeza kwenye viwanda vya kuchakata samaki na mnyororo wake wa thamani ili kukidhi uwezo wa viwanda hivyo.

Mhe. Dkt. Kijaji ameyasema hayo Disemba 23, 2024 alipotembelea kiwanda cha kuchakata samaki cha Pride of Nile PVT Ltd kilichopo katika Wilaya ya Muleba, Mkoani Kagera ambapo amebainisha kuwa uwekezaji huo ni matunda yanayotokana juhudi za Serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, za kuimarisha mazingira bora na wezeshi sambamba na kuhamasisha sekta binafsi kupanua wigo wa kuongeza thamani ya mazao ghafi ya sekta za uzalishaji, ikiwemo uvuvi.
"Jukumu letu kama Watanzania kwa sasa ni kuzilinda rasilimali hizi za asili kwa wivu mkubwa sana kwa sababu mbali na kutupatia ajira na kipato kwa mtu mmoja mmoja, pia rasilimali hizi zinanufaisha uchumi wa nchi kwa ujumla"
Aidha, Mhe. Dkt. Kijaji ametoa rai kwa wananchi kuongeza nguvu kwenye ufugaji samaki kwa njia ya vizimba ili kupumzisha shughuli za uvuvi wa asili na kuwapatia nafasi samaki wa asili (wild fish) wazaliane vya kutosha, sambamba na kumuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuongeza kasi ya uhamaishaji wa ufugaji wa samaki kwa vizimba.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhe. Dkt. Abel Nyamahanga, amesema kuwa asilimia 70 ya eneo la Wilaya hiyo limezungukwa na maji ya Ziwa Victoria na hivyo kufanya sehemu kubwa ya wakazi wa Wilaya ya Muleba kuwa wavuvi jambo linalowafanya kuwa na kila sababu ya kulinda rasilimali za Ziwa hilo kwa nguvu kubwa.
Akisoma taarifa ya mchango wa kiwanda chao kwenye soko la ajira, Meneja Ubora wa kiwanda hicho, Bw. Hamza Mustapha amesema kuwa kiwanda hicho kimefanikiwa kuajiri Watanzania 125 ambapo pia wanachangia uchumi wa Taifa kwa kulipa mrabaha na kodi mbalimbali za Serikali.
Comments