top of page

NI VITUKO WAGOMBEA UJUMBE MKUTANO MKUU BAVICHA, WASHINDWA KUJIELEZA, KUJIBU MASWALI

Na VENANCE JOHN

Vituko vimeshuhudiwa kutoka kwa wagombea wa ujumbe wa mkutano mkuu katika Baraza la Vijana la chama cha Chadema (Bavicha), Zanzibar na Bara kufuatia baadhi yao kushindwa kujieleza vema, kukosa sera na hata kushindwa kujibu maswali huku wengine wakitoa majibu ambayo yanaonekana kama ya mzaha yasiyo na umakini.


Mmoja wa wagombea ujumbe wa mkutano mkuu BAVICHA, upande wa Zanzibar, Alawiya Shaibu Hussein hakuwa na muda wa kumwaga sera, kwani baada ya kujitambulisha aliishia kusema anaomba kura.


Na ilipofika wakati wa kujibu maswali, aliulizwa iwapo atakusanya maswali yote ndipo ajibu, lakini yeye alijibu kwa kumwambia msimamizi wa uchaguzi "wewe endelea," bila kujibu swali.


Kama ilivyokuwa kwa swali la kwanza, mgombea huyo alishindwa kujibu, licha ya kuomba lirudiwe. Alipoulizwa swali la tatu atakifanyia nini chama hicho iwapo atachaguliwa amejibu, "kuhamasisha na kuhamasisha vijana."


Ulipofika wakati wa mgombea mwingine wa nafasi hiyo, Najma Hemed Ali ameanza kwa kujitambulisha jina na nafasi aliyonayo sasa, kisha akanyamaza kwa sekunde kadhaa, hivyo kusababisha minong'ono kutoka kwa wajumbe.


Msimamizi wa uchaguzi alipowataka wajumbe wawe watulivu, mgombea huyo alianza upya kujieleza kwa kusema, "Ni mjum.... Vijana naomba kura zenu." Ameendelea kwa kuwahoji wajumbe, "mmekubali au, kweli? Haya Asante."

Hayo yalisababisha vicheko kutoka kwa wajumbe wa mkutano huo wa uchaguzi.


Alipoulizwa swali la kwanza, Najma alikaa kimya, vivyo hivyo kwa swali la pili na tatu. Miongoni mwa wagombea waliotia mbwembwe katika kumwaga sera zake ni Pascal Mlapa anayeutaka ujumbe baraza kuu Bavicha, Bara.


Ameanza kwa kuitambulisha taaluma yake ya ujenzi wa maghorofa, akiihusisha na kile alichosema kama anajenga maghorofa hawezi kushindwa kujenga hoja. Sambamba na hilo, ameahidi kuhakikisha anakitibu kile alichokiita malaria iliyopo ndani ya chama hicho, kwa kusimamisha nguvu ya umma.


Kwa upande wa Barnaba Samwel anayegombea nafasi hiyo, amejinadi kwa kutaja nyadhifa mbalimbali alizowahi kushika na wingi wa nyadhifa alizowahi kushika, umesababisha swali kwamba amewahi kufanya nini katika nafasi hizo? Naye akajibu kuwa kwa sasa yeye ni mkunja ngumi kama wakunja ngumi wengine.


Uchaguzi wa Bavicha Tiafa umefanyika katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo Jumanne Januari 14, 2025.

Comments


Msasa Media
  • Instagram
  • Facebook
  • X
  • Youtube
  • TikTok

Follow, like, comment, and share

Tel. +255758379300
Mbezi Dar es saalam

bottom of page