Na VENANCE JOHN
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi akizungumza wakati akijibu swali leo Jumanne Januari 4, 2025 bungeni jijini Dodoma. Serikali imeanzisha riba kwa mifuko ya hifadhi ya jamii itakayosababisha ucheweshaji wa mafao kwa wanachama ambapo Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ukilipa asilimia 15 wakati Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) utalipa asilimia 5.
![](https://static.wixstatic.com/media/57c8da_e47ee3a52f2b4d9880e7d083ea4b7567~mv2.jpeg/v1/fill/w_980,h_980,al_c,q_85,usm_0.66_1.00_0.01,enc_avif,quality_auto/57c8da_e47ee3a52f2b4d9880e7d083ea4b7567~mv2.jpeg)
Hayo yamesemwa leo bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi alipokuwa akijibu swali la msingi la mbunge wa viti maalumu (CCM), Fakharia Shomar Khamis. Fakharia amehoji iwapo mstaafu aliyecheleweshewa kupata mafao anaweza kudai fedha kutokana na usumbufu alioupata wakati anasubiri mafao yake.
Akijibu swali hilo, Katambi amesema Sheria za NSSF na PSSSF katika vifungu 49(3) na 43(3) mtawalia, vinaeleza endapo mfuko utachelewesha kulipa mafao kwa mwanachama na uchelewesho huo haukusababishwa na mwanachama mwenyewe au mwajiri, utalipa riba. Amesema sheria imetoa haki ya mwanachama kulipwa fidia endapo atacheleweshewa kulipwa mafao yake ikiwa ucheleweshaji huo umesababishwa na mfuko.
Katika maswali ya nyongeza, Fakharia amehoji ni sababu gani za msingi ambazo zinasababisha mafao kuchelewa. Akijibu swali hilo, Katambi amesema moja ya changamoto iliyokuwepo awali ni wastaafu kuombwa nyaraka mbalimbali ikiwamo barua za kuajiriwa ambazo kimsingi zilitakiwa mwajiri kuwa nazo.
Comments