Na VENANCE JOHN
Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema, nchi za Magharibi zinaendelea kufanya mambo kana kwamba ni wawakilishi wa Mungu duniani kwa kujaribu kudumisha ukiritimba wao wa kimataifa kwa kuweka kanuni za kidanganyifu.

Akizungumza katika mkutano wa maafisa wakuu wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi, Putin amesema kuwa hali ya kijeshi na kisiasa duniani bado tata na tete, akiashiria umwagaji damu unaoendelea katika Mashariki ya Kati na maeneo mengine ya dunia.
Putin amefafanua kuwa, utawala wa sasa wa Marekani, pamoja na serikali nyingine nyingi za Magharibi, zingali zinajaribu kulinda na kuendeleza ukiritimba wao wa kimataifa na kulazimisha jamii ya kimataifa ifuate kanuni zao ambazo hubadilika na kupindishwa kila mara kwa namna inayowaridhisha wao. Putin amesema kuna wale wanaojiona kuwa wakuu wa ulimwengu wote, wale wanaojiona kuwa ni wawakilishi wa Mungu duniani, japokuwa wao wenyewe hawamwamini Mungu.
コメント