Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amesema utekelezaji wa mradi wa Bwawa la Kidunda utakapokamilika utaibua fursa nyingi za kimaendeleo ndani na nje ya Mkoa huo ambao hadi sasa utekelezaji wake umefikia Asilimia 27.8
![](https://static.wixstatic.com/media/57c8da_105ca2ed0f334d8db37efe59fc184778~mv2.jpeg/v1/fill/w_980,h_980,al_c,q_85,usm_0.66_1.00_0.01,enc_avif,quality_auto/57c8da_105ca2ed0f334d8db37efe59fc184778~mv2.jpeg)
Mradi wa ujenzi wa Bwawa la Maji Kidunda unaogharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 336 utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Juni 18, 2023 hadi Disemba, 2026, ukitekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Maji na kusimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA).
Jumanne ya Februari 4, 2025, Mhe. Malima amefanya Kikao baina yake na DAWASA iliyoongozwa na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Mhandisi Mkama Bwire kwa lengo la kupokea taarifa ya maendeleo ya mradi.
"Mradi huu ni muhimu sana kwakuwa utachochea fursa nyingi za maendeleo mkoani hapa, maendeleo ya miundombinu ya barabara toka Ngerengere hadi Kidunda umbali wa Km 75, Uzalishaji Umeme, Uboreshaji huduma ya Majisafi kwa vijiji vinavyopitiwa na Mradi, sambamba na kutoa ajira kwa wananchi wa Kidunda na maeneo jirani," amesema Mhe. Malima.
Kwa upande wake, Mhandisi Bwire ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 336 na kuridhia kuanza kwa utekelezaji wa mradi huu muhimu utakaoenda kuboresha upatikanaji huduma ya maji katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Miongoni mwa wadau walioshiriki kikao hicho ni pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe Musa Kilakala, Taasisi za Bonde la Wami-Ruvu, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Morogoro.
Kommentarer