Na VENANCE JOHN
Cristiano Ronaldo ameongoza tena orodha ya wanamichezo wanaolipwa pesa nyingi zaidi duniani na mapato ya jumla ya dola milioni 260 kwa mwaka 2024. Hii ni kulingana na tovuti ya habari za michezo ya Sportico, na katika orodha hiyo hakukuwa na hata mwanamke aliyepenya katika orodha hiyo ya wanamichezo 100 bora.

Sportico imesema mshambuliaji huyo wa Ureno, ambaye alisherehekea siku yake ya kuzaliwa ya 40 wiki iliyopita, alipata mshahara mnono wa dola milioni 215 huku pia akipata matangazo ya kibiashara ya dola milioni 45. Orodha ya wachezaji 100 wanaoongoza, kwa kiasi kikubwa imetawaliwa na wachezaji wa soka, NBA, NFL, gofu na ndondi.
Mkataba mzuri wa Ronaldo na timu ya soka ya Saudi Arabia ya Al-Nassr ulimhakikishia kubaki kileleni kwa mwaka wa pili mfululizo baada ya kuhamia ligi kuu ya Saudi Pro League Desemba 2022. Mlinzi wa Golden State Warriors, Stephen Curry, ambaye ni pili kwenye orodha hiyo. Nyota huyo wa NBA alipata dola milioni 153.8 mwaka 2024.
Bondia wa Uingereza Tyson Fury, ambaye alishindwa na Oleksandr Usyk wa Ukraine katika pambano la uzito wa juu mwezi Desemba, anashika nafasi ya tatu kwenye orodha akiwa na dola milioni 147.
Nafasi tano bora zinakamilishwa na nahodha wa Inter Miami kutoka Argentina Lionel Messi kwa kupata dola milioni 135 na fowadi wa Los Angeles Lakers, LeBron James kwa kupata dola milioni 133.2. Orodha ya 100 bora inaundwa na wanamichezo wanaocheza michezo minane tofauti na kutoka nchi 27.
Comments