Na VENANCE JOHN
Wakuu wa nchi kutoka Jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika SADC na wale wa jumuiya ya Afrika Mashariki, siku ya Ijumaa na Jumamosi ya wiki hii watakutana jijini Dar es Salaam, Tanzania, kuzungumzia mzozo unaoendelea kutokota mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
![](https://static.wixstatic.com/media/57c8da_2772b2b4c8ca4efeb6aa6fcfda0006cc~mv2.jpeg/v1/fill/w_980,h_980,al_c,q_85,usm_0.66_1.00_0.01,enc_avif,quality_auto/57c8da_2772b2b4c8ca4efeb6aa6fcfda0006cc~mv2.jpeg)
Mkutano huu ambao umethibitishwa na rais wa Kenya, William Ruto, ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, unakuja siku chache tu kupita tangu viongozi wa jumuiya hizo kwa nyakati tofauti wakubaliane kuwa na mkutano wa pamoja.
Katika mkutano huu, inatarajiwa kuwa rais wa Rwanda, Paul Kagame na mwenzake wa DRC, Felix Tshisekedi, watahudhuria, ambapo ikiwa watafanya hivyo itakuwa ni mara ya Kwanza kukutana ana kwa ana tangu kundi la M23 lichukue mji wa Goma.
Katika kikao cha wakuu wa nchi za Afrika Mashariki kilichofanyika juma moja lililopita kwa njia ya mtandao, rais Tshisekedi hakuhudhuria jambo lililoibua maswali ikiwa yuko tayari kwa mazungumzo ya kusaka suluhu ya kudumu kati yake na Kagame.
Aidha mkutano huu unaenda kufanyika wakati ambapo waasi wa M23 wanaosaidiwa na Rwanda, wakidhibiti maeneo ya mji wa Goma na sasa wanajaribu kuelekea Bukavu mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini.
Comments