top of page

TANZANIA, SAUDI ARABIA KUIMARISHA USHIRIKIANO SEKTA YA NISHATI

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Saudi Arabia katika kuimarisha Sekta ya Nishati hususan katika Mafuta na Gesi, Nishati Safi ya Kupikia na Nishati Jadidifu.


Mhe. Kapinga amesema hayo wakati alipokutana na Naibu Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia, Mhandisi Mohammed Albrahim katika Mji wa Riyadh tarehe 19 Desemba, 2024 nchini Saudi Arabia.


Amesema kuwa, Tanzania imekuwa ikishirikiana na nchi hiyo kwa muda mrefu katika Biashara ya Mafuta na Maeneo Mengine ya Maendeleo hivyo mahusiano hayo yanaendelea kuimarika zaidi kwa kuwa mahitaji ya nishati yanazidi kuongezeka na uwekezaji zaidi unahitajika katika kuendeleza Sekta ya Nishati ikiwemo Mafuta na Gesi Asilia, Nishati Jadidifu na Nishati Safi ya Kupikia.


"Mahusiano ya Tanzania na Saudi Arabia katika Sekta ya Nishati ni ya muda mrefu, nchi hizi mbili zimekuwa na lengo la kuboresha ushirikiano wao katika kuendeleza sekta ya nishati." Amesema Kapinga


Aidha, ameeleza kuwa Tanzania kama nchi inayoendelea inahitaji kuimarisha zaidi miundombinu yake ya nishati katika maendeleo hivyo imekuwa ikishirikiana na nchi zenye uzoefu mkubwa katika sekta hizo ili kupata matokeo chanya kwa kuwa nishati ni msingi mkuu wa maendeleo.


Amesema Saudi Arabia imekuwa ikijulikana kwa uwezo wake mkubwa katika uzalishaji wa mafuta na gesi, na imekuwa ikiwekeza katika maeneo mbalimbali ya Dunia, ikiwemo Afrika Mashariki, ambapo kwa upande wa Tanzania yenye rasilimali za Gesi Asilia na viashiria vya uwepo wa Mafuta inapata uzoefu, ujuzi na teknolojia kutoka Saudi Arabia katika kuchimba, kusafisha na kusafirisha mafuta na gesi pamoja na kuimarisha miundombinu ya rasilimali hizo.

Comments


Msasa Media
  • Instagram
  • Facebook
  • X
  • Youtube
  • TikTok

Follow, like, comment, and share

Tel. +255758379300
Mbezi Dar es saalam

bottom of page