top of page

TBA KUSIMAMIA UKARABATI WA UWANJA WA UHURU....

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) utasimamia ukarabati wa uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam ambao utafanywa na Mkandarasi CRCEG kutoka China. Hatua hiyo imekuja baada ya



Kampuni hiyo kuingia Mkataba na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Aprili 25, 2024.

Akizungumza wakati wa utiaji saini wa mkataba huo Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Gerson Msigwa amesema nchi yetu imepata fursa ya kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa ya AFCON pamoja na Kenya na Uganda ambapo kwa upande wa Tanzania tunaendelea na ujenzi na ukarabati wa viwanja vyetu ili kuweza kujiandaa kikamilifu na mashindano hayo.

Aidha, Msigwa amesema kwa hatua hiyo leo tumeshuhudia utiaji saini mkataba wa ukarabati mkubwa wa uwanja wa Uhuru ambapo zoezi zima la ukarabati litachukua kipindi cha miezi kumi na mbili (12).

Vile vile Msigwa amezipongeza TBA na Kampuni ya CRCGE kwa kuingia mkataba na Wizara kwa ajili ya ukarabati wa uwanja huo.

Awali akizungumza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Suleiman Serera amesema kuwa ukarabati huo utagharimu fedha kiasi cha bilioni 19.7 ambapo ukarabati huo utajumuisha ukarabati wa miundombinu ya eneo la kuchezea (pitch), eneo la kukaa watu, mifumo ya maji safi na maji taka, viyoyozi, sauti pamoja na kubadili milango na madirisha.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Ushauri wa TBA Arch. Victor Balthazar amesema timu ya wataalamu kutoka TBA imejipanga kuhakikisha inasimamia ukarabati wote utakaokwenda kufanyika sambamba na kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa na Serikali juu ya kuongeza idadi ya watu kufikia elfu thelathini.

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) iliingia Mkataba na Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo Februari 2023 kwa ajili ya kusimamia ukarabati wa viwanja saba nchini vikiwepo viwanja vya Uhuru na Benjamini Mkapa vilivyopo jijini Dar es Salaam.

Comments


Msasa Media
  • Instagram
  • Facebook
  • X
  • Youtube
  • TikTok

Follow, like, comment, and share

Tel. +255758379300
Mbezi Dar es saalam

bottom of page