top of page

TEWW YADURUSU MODULI ZA ELIMU YA SEKONDARI ILI KUENDANA NA MAHITAJI YA SOKO

Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) mwishoni mwa wiki hii imekamilisha kazi ya kudurusu moduli za elimu ya Sekondari nje ya mfumo rasmi ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira nchini.


Maandalizi hayo yaliyochukua takriban wiki mbili (2) na kuwashirikisha wataalamu kutoka TEWW na wadau wa elimu kutoka taasisi mbalimbali za elimu nchini yamefanyika katika kituo cha TEWW mjini Morogoro.


Kwa mujibu wa Mratibu wa mradi wa kuboresha elimu ya Sekondari kwa njia mbadala (SEQUIP-AEP), Bw. Baraka Kionywaki, TEWW imeamua kuboresha moduli za kufundishia wanafunzi wanaosoma kwa njia mbadala ili ziendane na Sera ya Elimu ya Mwaka 2014, toleo la 2023 inayotarajiwa kuzinduliwa mwishoni mwa Mwezi huu jijini Dodoma.


“Kupitia Sera ya Elimu, tamko Na. 3.5.1.1 na 3.5.1.2, Serikali kwa kushirikiana na wadau itaweka mazingira wezeshi ili kuhakikisha elimu ya watu wazima na endelevu inatolewa kwa ufanisi katika ngazi zote kwa njia mbalimbali, ikiwemo huria na masafa," Bw. Kionywaki alisema, na kuongeza kuwa lengo la hatua hiyo ni kuwapa Watanzania ari ya kujiendeleza.


Kwa upande wake, Mkuza Mitaala kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Bw. Nehemia Kaaya, ameipongeza TEWW kwa juhudi zake za kudurusu moduli kwa kuzingatia viwango vya ubora na kwa azma yake ya kuwaandaa wanafunzi kuwa na umahiri wa utendaji kazi. “Zoezi hili linalenga kuhakikisha elimu inayotolewa inawapa wanafunzi uwezo wa kukidhi mahitaji ya sasa ya soko la ajira na maisha ya kila siku ya Mtanzania,” Bw. Kaaya alisema.


Zoezi la kudurusu moduli limefanyika katika hatua mbili (2); hatua ya kwanza ikihusisha masomo ya Kidato cha I na II, na hatua ya pili Kidato cha III na IV. Moduli hizo zinahusu masomo ya Historia, Jiografia, Kiswahili na Baiolojia.

Pia, masomo ya Kemia, Fizikia, Kiingereza na Hisabati.


Kazi hii ya kudurusu moduli imefanyika chini ya mradi wa SEQUIP-AEP unaotekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo kupitia Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima.

Comments


Msasa Media
  • Instagram
  • Facebook
  • X
  • Youtube
  • TikTok

Follow, like, comment, and share

Tel. +255758379300
Mbezi Dar es saalam

bottom of page