top of page

URUSI YAMKAMATA MSHUKIWA WA MAUAJI YA JENERALI MKUU KITENGO CHA SILAHA ZA NYUKLIA NA KEMIKALI

Na VENANCE JOHN


Urusi leo imesema kuwa inamshikilia raia wa Uzbekistan ambaye amekiri kutega na kulipua bomu lililomuua Luteni Jenerali Igor Kirillov mjini Moscow hapo jana na kwamba alifanya hivyo kwa maagizo ya idara ya usalama ya Ukraine.


Kamati ya Upelelezi ya Urusi, ambayo inachunguza uhalifu mkubwa, imesema katika taarifa yake siku ya leo kwamba mshukiwa ambaye hakutajwa jina aliwaambia kwamba alikwenda jijini Moscow kutekeleza jukumu la idara ya ujasusi ya Ukraine.


Katika video ya kukiri hilo iliyochapishwa na kituo cha habari cha Baza, ambacho kinajulikana kuwa na vyanzo katika duru za sheria za Urusi, mshukiwa anaonekana ameketi kwenye gari akielezea matendo yake.


Akiwa amevalia koti la majira ya baridi, mshukiwa anaonyeshwa akisema alikuja Moscow kwa amri ya idara ya ujasusi ya Ukraine, akanunua baiskeli ya umeme, kisha akapokea kilipuzi kilichoboreshwa kutekeleza mlipuko huo miezi kadhaa baadaye.


Wachunguzi wamesema kwamba mtuhumiwa alikuwa ameweka kamera ya uchunguzi katika gari la kukodi karibu na kwamba waandaaji wa mauaji hayo, walikuwa katika mji wa Dnipro, nchini Ukraine, na walitumia kamera hiyo kutazama kile kinachotokea.


Anasema Ukraine ilikuwa imempa dola 100,000 kwa jukumu lake katika mauaji na ukaazi katika nchi moja ya Ulaya. Wachunguzi walisema walikuwa wakiwatambua watu wengine waliohusika na tukio hilo na gazeti la kila siku la Kommersant liliripoti kuwa mshukiwa mwingine mmoja amekamatwa.


Igor Kirillov, ambaye alikuwa mkuu wa Kikosi cha Kulinda silaha za Nyuklia, Biolojia na Kemikali cha Urusi, aliuawa nje ya jengo lake la ghorofa pamoja na msaidizi wake wakati bomu lililofichwa kwenye baiskeli ya umeme lilipolipuka.


Alikuwa afisa mkuu wa jeshi la Urusi kuuliwa na Ukraine ndani ya Urusi. Idara ya kijasusi ya Ukraine SBU, mara kwa mara ilkuwa ikimshutumu Igor Kirillov kwa kuhusika na matumizi ya silaha za kemikali dhidi ya wanajeshi wa Ukraine, jambo ambalo Urusi ilikuwa mara zote ikikanusha.

Comments


Msasa Media
  • Instagram
  • Facebook
  • X
  • Youtube
  • TikTok

Follow, like, comment, and share

Tel. +255758379300
Mbezi Dar es saalam

bottom of page