top of page

WAASI WA M23 WASEMA LENGO NI KUMPINDUA RAIS TSHISEKEDI, SASA KUSONGA MBELE KUISAKA KINSHASA

Na VENANCE JOHN


Kiongozi wa waasi wa M23, Corneille Nangaa ambaye wapiganaji wake wameuteka mji wa Goma, mji mkubwa zaidi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ameapa kuendelea na mashambulizi hadi mji mkuu wa Kinshasa. Corneille Nangaa, ambaye anaongoza muungano wa makundi ya waasi ambayo yanajumuisha M23, amesema lengo lao kuu ni kupindua serikali ya Rais Félix Tshisekedi.


Taarifa ambazo bado hazijathibitishwa kwa sasa zinasema kuwa waasi hao kwa sasa wanasonga mbele kuelekea Bukavu, jiji la pili kwa ukubwa katika eneo la mashariki lenye utajiri wa madini, licha ya wito wa kimataifa wa kusitisha mapigano. Katika hotuba ya runinga baada ya Goma kushikiliwa na waasi, Rais Felix Tshisekedi alisema mwitikio wa nguvu na ulioratibiwa ulikuwa unaendelea ili kurejesha udhibiti wa Goma.


"Tunawahakikishia jambo moja; Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo haitaruhusu kufedheheshwa au kupondwa. Tutapigana na tutashinda," Rais Tshisekedi alisema. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mapigano hayo yamewalazimu takribani watu 500,000 kuondoka kwenye makazi yao, na kuzidisha hali mbaya ya kibinadamu.


Hapo jana kiongozi wa muungano wa makundi ya waasi likiwemo M23 linaloungwa mkono na Rwanda aliwatambulisha waasi hao kama wasimamizi wapya wa Goma, akiwaambia waandishi habari kwamba ndio wamekita mizizi katika eneo hilo. Tangu mapigano yalipoongezeka wiki iliyopita, umeme na usambazaji wa maji katika jiji hilo umekatika, na chakula ni kichache.

Comments


Msasa Media
  • Instagram
  • Facebook
  • X
  • Youtube
  • TikTok

Follow, like, comment, and share

Tel. +255758379300
Mbezi Dar es saalam

bottom of page