Na VENANCE JOHN
Jeshi la Ghana limesema wachimba madini haramu saba wameuawa katika ufyatulianaji wa risasi katika eneo la Ashanti nchini humo.
![](https://static.wixstatic.com/media/57c8da_c45804407db7420cb7054f1aeae4b7c5~mv2.jpeg/v1/fill/w_980,h_980,al_c,q_85,usm_0.66_1.00_0.01,enc_avif,quality_auto/57c8da_c45804407db7420cb7054f1aeae4b7c5~mv2.jpeg)
Mauaji hayo yamesababisha maandamano ya umma katika mji wa Obuasi ambako mabasi kadhaa yamechomwa moto. Kulingana na jeshi la Ghana, takriban watu sitini wenye silaha walivunja uzio wa usalama kwenye mgodi unaosimamiwa na kampuni ya AngloGold Ashanti.
Taarifa inasema, askari walipojaribu kuwazuia watu hao, walifyatuliwa risasi. Hilo si tukio la kwanza kwani mwezi Septemba kampuni nyingine ya uchimbaji madini katika eneo hilo hilo ilisema imekuwa ikivamiwa mara kwa mara na magenge ya watu wenye silaha.
Kumekuwa na ongezeko la uchimbaji madini haramu kote nchini Ghana ambako kumechochewa na ugumu wa maisha na uchumi wa nchi hiyo kudorola kwa kiasi kinachotajwa kuwa hakikuwahi kushuhudiwa katika kizazi cha sasa.
Comments