top of page

WATATU WASHIKILIWA NA POLISI AKIWEMO MTOTO ANAYEDAIWA KUIBA WATOTO SITA

Na VENANCE JOHN


Jeshi la Polisi limesema kuwa linawashikilia watu wawili waliosikika kwenye video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii wakimhoji mtoto aliyejitambulisha kwa jina la Evaristo.


Pia, jeshi la polisi linamshikilia mtoto huyo ili kuendelea na uchunguzi wa maelezo yaliyozungumzwa na mtoto huyo katika kipande hicho cha video akijinasibu kwa wizi wa watoto.


Taarifa ya kushikiliwa kwa watu hao imetolewa leo Jumatatu Agosti 26, 2024 na msemaji wa jeshi hilo, David Misime. Katika kipande hicho cha video, mtoto huyo alisikika akijinasibu kwa wizi wa watoto akishirikiana na wenzake watatu kwa kuwarubuni kwa pipi.


“Nimeshateka watoto sita hadi sasa, wameshakufa,” alisikika mtoto huyo akihojiwa na watu wawili ambao zilisikika sauti zao kwenye video hiyo. Kwa mujibu wa Misime, katika taarifa hiyo aliyetajwa kuwa mshirika wa mtoto huyo kwenye wizi huo wa watoto naye amekamatwa.


“Aliyemtaja kwamba akishaiba watoto wadogo akishirikiana na wenzake humkabidhi na yeye huwaua, kisha kuwafunga kwenye maboksi na kuwasafirisha hadi Dar es Salaam, askari wamefanikiwa kumpata,” ameeleza Misime.


Misime amesema pia jeshi hilo lilifika Kitongoji cha Nero wilayani Chalinze ambako mtoto huyo anadai kuiba watoto sita na baada ya mahojiano na viongozi mbalimbali, haijathibitika kupotea kwa mtoto yeyote.


Misime amewaondoa hofu wananchi kuhusu video hiyo na kusisitiza kwamba haijathibitika mpaka sasa kwamba kilichozungumzwa ni uhalisia. Misime amesema uchunguzi wa awali unaonesha mtoto huyo pamoja na wenzake wanatuhumiwa kujihusisha na wizi wa nguo na vitu vingine katika maeneo mbalimbali.


Comments


Msasa Media
  • Instagram
  • Facebook
  • X
  • Youtube
  • TikTok

Follow, like, comment, and share

Tel. +255758379300
Mbezi Dar es saalam

bottom of page