Na Ester Madeghe,
Vikosi vya Ulinzi vya Yemen vimetangaza kuwa vimezishambulia meli tatu kwa kukiuka marufuku iliyowekwa na nchi hiyo ya kupita kwenye eneo la maji yake kuelekea bandari za utawala wa Israel katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu. Msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Yemen Brigedia Jenerali Yahya Saree ametoa taarifa hiyo jana kupitia televisheni.

Saree amesema: "meli ya SC Montreal ililengwa na ndege mbili zisizo na rubani kusini mwa Bahari ya Arabia" na akaongeza kuwa, meli nyingine iliyotambuliwa kama Maersk Kowloon, ililengwa katika Bahari ya Arabia kwa kombora la kruzi. Kwa mujibu wa msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Yemen, meli nyingine ya Motaro ililengwa katika Bahari Nyekundu na Bab al-Mandab kwa makombora kadhaa ya balestiki.
Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema, Shirika la Uingereza la Operesheni za Biashara ya Baharini (UKMTO), limeripoti kuwa kuna meli ambayo imeshambuliwa umbali wa maili 25 kusini mwa mji wa bandari wa al-Mukha katika Bahari Nyekundu kusini magharibi mwa Yemen. Hayo yanajiri, mara baada ya jeshi la Israel kuanzisha mashambulizi katika ukanda wa Gaza, hali inayofanya baadhi ya mataifa ya Kiislamu kuishambulia Israel, kama ishara ya kulipa kisasi.
Comments